KFCB yapeleka elimu kuhusu vyombo vya habari Nyeri

Wadau walielimishwa kuhusu uundaji na matumizi yanayowajibika ya maudhui, huku wakiangazia hatua za udhibiti zinazolenga kuimarisha sekta hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read

Bodi ya Kuainisha Filamu ya Kenya, KFCB, kwa kuzingatia jukumu lake la kutoa ushauri kwa watumiaji na dhamira yake ya kushirikiana na wadau, ilipeleka elimu ya uelewa wa vyombo vya habari katika kaunti ya Nyeri.

Wanachama wa bodi hiyo walikutana na wabunifu pamoja na wanaotumia maudhui ya sauti na picha wakati wa shughuli ya siku ya Maskauti na Utalii ya Nyeri iliyofanyika katika uwanja wa Kamukunji.

Wadau hao walielimishwa kuhusu uundaji na matumizi yanayowajibika ya maudhui, huku wakiangazia hatua za udhibiti zinazolenga kuimarisha sekta hiyo.

Zaidi ya uhamasishaji wa umma, KFCB inatekeleza hatua zinazorahisisha michakato ya udhibiti, kujenga uwezo wa sekta na kupanua upatikanaji wa maudhui na fursa.

Hatua hizo zinajumuisha Mfumo wa Uainishaji wa Kujitegemea, utoaji wa leseni kidijitali kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Kiufundi na jukwaa la eCitizen, kufafanuliwa upya kwa jukumu la Mawakala wa Filamu pamoja na kituo cha filamu cha Nairobi na kituo tamba cha filamu.

Hatua hizi zote zinalenga kusaidia ukuaji na maendeleo ya sekta ya maudhui ya sauti na picha.

Timu ya KFCB pia ilimkaribisha Kang Hyung-shik, Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Kenya, pamoja na Mutahi Kahiga, Gavana wa Kaunti ya Nyeri, ambao walitembelea banda la maonyesho la Bodi.

Ziara hiyo ilisisitiza dhamira ya KFCB ya kushirikiana na wadau katika kujenga mazingira wezeshi ya udhibiti yanayounga mkono sekta imara na yenye uhai ya maudhui ya sauti na picha.

Share This Article