Maafisa wa Polisi nchini Uganda, wameanzisha uchunguzi wa mauaji ya mwanamuziki mkongwe na kiongozi wa bendi ya Afrigo, Moses Matovu, aliyeshambuliwa huko Kibuli, Kampala.
Msemaji wa Polisi wa eneo la jiji la Kampala, Rachael Kawala, alisema kuwa watu wasiojulikana walimshambulia Matovu asubuhi ya Septemba 24, 2026, katika Eneo B la Soko la Kibuli, Wilaya ya Makindye.
Ripoti zinaeleza kuwa washambuliaji walimpiga kichwani na kusababisha apoteze damu nyingi. Alikimbizwa katika Hospitali ya Kibuli, ambako baadaye alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata.
Kawala alisema Polisi wa Kabalagala walikuwa wamefungua kesi hiyo kama mauaji yanayoshukiwa. Wachunguzi pia walizuru eneo la tukio ili kubaini mazingira yaliyosababisha shambulio hilo.
“Kikosi chetu cha uchunguzi kwa sasa kiko katika eneo la tukio kikifanya uchunguzi ili kubaini mazingira ya tukio hilo. Juhudi pia zinaendelea kuwabaini na kuwakamata washukiwa wa shambulio hilo,” Kawala alisema.
Polisi hawajafichua idadi ya washambuliaji, silaha iliyotumika wala sababu inayodhaniwa kuwa chanzo cha shambulio hilo. Hakuna taarifa ya kukamatwa kwa mtu yeyote kufikia sasa.
Wanachama kadhaa wa bendi ya Afrigo kama Joanita Kawalya na Racheal Magoola tayari wamefika katika msikiti wa Kibuli kumwomboleza Moses Matovu.