Benki Kuu ya Kenya, CBK imeidhinisha uhamisho wa mali na madeni yote ya benki ya Access nchini Kenya kwenda kwa benki ya National, NBK.
Haya yametekelezwa katika shughuli inayotarajiwa kuimarisha ushindani na ustahimilivu katika sekta ya benki.
CBK ilisema uhamisho huo uliidhinishwa Agosti 17, 2026, chini ya Sheria ya Benki, huku Waziri wa Fedha na Mipango ya Kitaifa akiidhinisha shughuli hiyo Septemba 21.
Uhamisho huo utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa taratibu kwa mujibu wa Mkataba wa Uhamisho wa Biashara na Mali uliotiwa saini kati ya benki hizo mbili.
NBK, iliyoanzishwa mwaka 1968 kama taasisi inayomilikiwa na serikali, ilinunuliwa na KCB Group mwaka 2019. Access Bank Plc baadaye ilinunua asilimia 100 ya hisa zilizotolewa za NBK kutoka KCB Group mwezi Mei 2025.
Access Bank iliingia katika soko la Kenya Februari 2020 kupitia ununuzi wa Transnational Bank Plc, ambayo ilianza shughuli zake mwaka 1985.
Access Bank yenye makao yake Nigeria ni kampuni tanzu ya Access Holdings Plc na inaendesha shughuli katika masoko kadhaa ya Afrika, pamoja na Uingereza, China, India, Lebanon na Falme za Kiarabu.
CBK ilisema shughuli hiyo itasaidia kudumisha uthabiti, kuimarisha ustahimilivu na kukuza ushindani katika sekta ya benki nchini Kenya.