Kinyang’anyiro cha katibu mkuu UN: Michelle Bachelet ajindondoa

Uamuzi wake ulifuatia kura ya tatu ya maoni isiyo rasmi ya Baraza la Usalama la UN iliyofanyika Ijumaa.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa zamani wa Chile, Michelle Bachelet amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kuwa Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa, UN.

Hatua hii inafikisha kikomo, azma yake ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza shirika hilo katika historia yake ya miaka 80.

Bachelet wa umri wa miaka 74, alitangaza uamuzi huo Jumamosi kupitia video kwenye Instagram, akisema hakujutia kukubali changamoto hii kubwa licha ya kuona kuwa huenda wakati haukuwa mwafaka kwa aina ya kampeni aliyotaka kuwakilisha.

Uamuzi wake ulifuatia kura ya tatu ya maoni isiyo rasmi ya Baraza la Usalama la UN iliyofanyika Ijumaa.

Bachelet alipata kura moja ya kuhimizwa, 11 za kutohimizwa na tatu za waliokosa maoni, ikilinganishwa na kura sita za kumuunga mkono Julai na mbili Agosti.

Rebeca Grynspan wa Costa Rica, mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Biashara na Maendeleo, UNTD, aliongoza kura hiyo kwa kura tisa za kumuunga mkono, akifuatiwa na Carolyn Rodrigues-Birkett wa Guyana aliyepata nane.

Wagombea wengine ni Rafael Grossi wa IAEA, Rais wa zamani wa Senegal Macky Sall na mwanadiplomasia wa Ecuador Maria Fernanda Espinosa.

Atakayemrithi Antonio Guterres, ambaye muhula wake unamalizika Desemba 31, ataongoza UN wakati shirika hilo linakabiliwa na changamoto za kifedha na migogoro ya kimataifa, ikiwemo Gaza na Ukraine.

Share This Article