Bunge la Nigeria limepiga marufuku ziara rasmi nchini Afrika, kama hatua ya kulalamikia ghasia ambazo zinawalenga raia wa kigeni, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya raia wa Nigeria.
“Ziara zote rasmi katika Jamhuri ya Afrika Kusini za Bunge la Taifa, kamati zake, wabunge, maafisa na wafanyakazi wake, zimepigwa marufuku mara moja,” ilisema taarifa ya msemaji wa bunge hilo Akin Rotimi leo Ijumaa.
Kulingana na taarifa hiyo, marufuku hiyo inajumuisha mikutano kupitia mtandaoni, ikijiri baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni nchini Afrika Kusini, ambayo yamesababisha maelfu ya raia wa kigeni kuondoka nchini humo.
“Bunge la Taifa haliwezi puuza mashmbulizi dhidi ya raia walio ugenini,” alisema Rotini.
Kwa upande wake, karani wa bunge la Nigeria Kamoru Ogunlana, alisema kupitia kwa taarifa kwamba bunge hilo linatilia maanani ripoti kwamba raia wa Nigeria wanauawa, kujeruhiwa, kuachwa bila makao na kulazimishwa kuacha biashara zao, uwekezaji, nyumba na mali zingine kutokana na mashambulizi hayo.
Maelfu ya raia wa kigeni wamelazimika kuondoka Afrika Kusini, kutokana na mashambulizi, huku nchi kadhaa zikijitahidi kuwahamisha raia wao wanaotaka kuondoka nchini humo kwa hiari.