Weasel amtaka Kid Fox kumheshimu Bobi Wine

Hii ni baada ya Kid Fox kujisingizia kutomfahamu kabisa mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Uganda Weasel Manizo ametoa ushauri kwa msanii mwenzake Kid Fox kuepuka kuwashambulia wasanii wenzake waliobobea, hasa Bobi Wine.

Weasel ambaye jina lake halisi ni Douglas Mayanja anasisitiza kwamba mambo mengi yamebadilika katika tasnia ya muziki ya nchini humo.

Akizungumza kwenye mahojiano ya hivi karibuni, Kid Fox, ambaye amerejea Uganda rasmi baada ya kukaa ughaibuni miaka mingi, alionekana kujisingizia kutomfahamu kabisa mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine.

Kauli zake zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, ambao walimtaka Kid Fox asimdharau mtu ambaye historia ya maisha yake imekuwa ikisifiwa kimataifa katika miaka ya hivi karibuni.

Weasel pia ameungana na waliomtaka Kid Fox atulie na kuwa na nidhamu.

Mwimbaji huyo wa kampuni ya Goodlyfe Music, alieleza kwamba Bobi Wine yuko katika kiwango chake mwenyewe na anastahili heshima kutoka kwa wasanii wote.

“Umekuwa mbali kwa muda mrefu sana, na sasa watu wanamiliki majumba makubwa na wanaendesha magari ya G-Wagon. Hata Weasel, ambaye ulimwacha akiwa hana kitu, sasa anamiliki V8 na jumba,” alisema Weasel.

Aliendelea kumshauri aelewe kwamba tasnia ni kama msitu wa zege akiongeza, “Acha kuwadharau Bebe Cool na Bobi Wine, hasa Bobi Wine, kwa sababu hayuko tena katika kiwango chetu. Mwachie; usimhusishe na matusi yako. Kama humjui vizuri, basi hata mama yako mwenyewe humjui.”

Share This Article