Katibu Kipronoh asema serikali inanuia kuiboresha sekta ya chai

Martin Mwanje
1 Min Read
Katibu Kipronoh Ronoh alipotembelea kiwanda cha Chelal Agosti 21, 2026

Katika katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh leo Ijumaa amekutana na wakulima wa majani chai katika kiwanda cha Chelal katika kaunti ya Kericho.

Ni wakati wa mkutano huo aliposisitiza dhamira ya serikali kuhakikisha sekta ya chai inakuwa ya kisasa, yenye ushindani na inayotoa kipaumbele kwa wakulima.

Chelal ni miongoni mwa viwanda 17 vilivyo katika awamu ya kwanza ya kufanywa kuwa vya kisasa.

 

Dkt. Kipronoh aliwasilisha msaada wa serikali wa shilingi milioni 51.2 ili kusaidia katika uboreshaji na uchakataji wa viwanda vya chai, na kisha kuzindua usambazaji wa mbegu za chai 10,000.

Aidha, ameiagiza Bodi ya Chai nchini Kenya, TBK kuimarisha uangalizi, kutokomeza ulaghai wa upimaji wa bidhaa hiyo na kuwezesha uanzishwaji wa vibanda vya chai katika vituo vya manunuzi.

Mfumo wa Dijitali wa Malipo ya Chai umepangwa kuanzishwa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kwa manufaa ya wakulima, ikiashiria dhamira ya serikali kuifanya sekta ya chai nchini kuwa ya kisasa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TBK Willy Mutai na mwenyekiti wa bodi hiyo Ndung’u Gathinji ni miongoni mwa waliokuwapo.

Share This Article