Mahakama Kuu imtenga Septemba 16, 2026, kuwa siku ambayo aliyekuwa Gavana wa Migori, Zachary Okoth Obado na wenzake wawili watajua adhabu watakazopata kwa mauaji ya Sharon Otieno.
Obado, aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori, Caspal Obiero watahukumiwa siku hiyo kuhusiana na mauaji ya mwanafunzi huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Rongo, mwaka 2018..
Tarehe ya hukumu ilithibitishwa leo Jumanne, Agosti 18, baada ya afisa wa uangalizi kuwasilisha ripoti ya athari kwa waathiriwa, iliyoeleza madhara ambayo mauaji ya Sharon yamesababishia familia yake.
Jaji Cecilia Githua aliagiza upande wa mashtaka na utetezi kuwasilisha na kubadilishana mawasilisho yao kuhusu adhabu kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo. Mahakama itazingatia ripoti ya athari kwa waathiriwa na mawasilisho hayo kabla ya kuamua adhabu inayofaa.
Julai 23, Jaji Githua aliwapata Obado, Oyamo na Obiero na hatia ya mauaji ya Sharon, akisema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake bila shaka yoyote kupitia ushahidi wa kimazingira uliounda mtiririko kamili wa matukio.
Mahakama ilibaini kuwa kila mmoja alitekeleza jukumu tofauti.
Familia ya Sharon imesema ilitumia takriban Sh4.7 milioni kufuatilia haki kwa karibu miaka minane, kiasi kilichowalazimu kuuza ardhi na ng’ombe.
Sasa familia hiyo inataka kufidiwa gharama hizo na kupatiwa gari na nyumba, vitu ambavyo Obado alikuwa amemuahidi Sharon.
Washtakiwa wote watatu wataendelea kuzuiliwa hadi Septemba 16, wakati mahakama itaamua adhabu zao.