Serikali inasema imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha usalama wa nchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo anasema serikali ina tajiriba ya kutosha ya kushughulikia masuala ya usalama kwa kutilia maanani ilivyoshughulikia chaguzi zilizopita.
“Tuna mpango mpana wa kimkakati ambao utaongoza upelekwaji wa maafisa wetu wa usalama kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na pia baada ya uchaguzi,” alisema Katibu Omollo wakati pirikapirika za uchaguzi mkuu ujao zikianza kushika kasi.
“Uzuri ni kwamba si mara ya kwanza kwa nchi hii kuandaa uchaguzi, hivyo tuna uzoefu mkubwa hata kwa kurejelea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 ambapo asasi zetu za usalama zilifanya kadiri ziwezavyo kwa kusaidiwa na wadau wengine ikiwa ni pamoja na washirika wa maendeleo.”
Kauli zake zinawadia wakati ambapo wanasiasa wa mirengo mbalimbali wameanza kuzuru maeneo mbalimbali ya nchi katika kile kinachoonekana kama jitihada za kuwinda kura.
Hii ni hata kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC kupuliza kipenga rasmi cha kampeni kuanza.
Tume hiyo inayoongozwa na Erastus Ethekon imetangaza kuwa kampeni rasmi zitaanza Mei 29 na kukamilika Agosti 7 mwakani.