Rais William Ruto leo Jumatano ameelezea sababu za ni kwa nini Kenya inahitaji mpango mpya wa maendeleo kupitia Ruwaza 2060.
Amesema Ruwaza 2030 ambayo muda wake unakamilika katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, ilitayarishwa katika mazingira tofauti kabisa ukilinganisha na wakati huu.
Aidha, Rais Ruto amesema ruwaza hiyo ilitayarishwa wakati ambapo Kenya haikuwa na katiba mpya, ikiwa na maana kwamba umma haukushirikishwa katika uundaji wake.
Kinyume cha ruwaza hiyo, Ruto amesema Ruwaza 2060 ni mradi wa watu wala si wa serikali wala wanateknokrasia.
“Huu si mradi wa serikali, ni mradi unaoendeshwa na watu,” alisema Rais wakati wa uzinduzi wa Ruwaza 2060 katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC, jijini Nairobi.
“Tunataka kupata maoni ya kila mtu, wakulima, sekta binafsi, wanafunzi, wanazuoni, na wanateknokrasia. Hakuna aliye na ukiritimba wa maarifa.”
Kiongozi wa taifa pia alielezea kuwa Ruwaza 2030 iliundwa wakati ambapo mabadiliko makubwa hayakuwa yametokea duniani, ikiwa na maana kwamba mabadiliko hayo hayakuzingatiwa katika mipango ya maendeleo ya taifa.
Alitoa mfano wa maendeleo ya teknolojia yaliyofikiwa duniani kama vile teknolojia ya akili unde, AI ambayo athari yake kwa ustawi wa dunia inaendelea kuhisiwa katika kila nyanja, na masuala kama vile mabadiliko ya tabia nchi.
Masuala ambayo alisisitiza yanapaswa kuzingatiwa katika uundaji wa mpango mpya wa maendeleo.