Tamasha ya miaka 30 ya Bongo Fleva kuelekea Dodoma

Hii ni baada ya tamasha hiyo kufanyika kwa mafanikio Jijini Mwanza Agosti 8, 2026.

Marion Bosire
1 Min Read

Kamati ya maandalizi ya tamasha za miaka 30 ya Bongo Flava nchini Tanzania, imetangaza kwamba onyesho hilo sasa linaelekea jijini Dodoma kwa ajili ya maadhimisho hayo, baada ya kufanyika kwa mafanikio Jijini Mwanza.

Taarifa iliyotolewa kwa niaba ya kamati hiyo na Hamadi Ally Seneda, inasema kwamba tamasha inayofuata itafanyika Agosti 22, 2026 katika uwanja wa Chinangali, Dodoma.

Wakati huo huo kamati imeshukuru washiriki na wadau mbalimbali waliofanikisha maadhimisho ya Mwanza, ikieleza kuwa lengo la sherehe hizo sio kutoa burudani pekee, bali pia kuwawezesha wasanii na wanajamii kiuchumi na kuimarisha uchumi wa ubunifu humu nchini.

Aidha, kamati andalizi imeelezea kwamba maadhimisho hayo yanalenga kuendelea kuuenzi na kutangaza urithi wa muziki wa Bongo Flava, huku safari hiyo ikiendelea katika Mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

Katika tamasha kuu jijini Dar es Salaam Julai 10, 2026, wanamuziki wa Kenya Nyota Ndogo na Jua Cali waliwakilisha huku CMB Prezzo akiwakilisha Kenya katika awamu ya Mwanza.

Akiwa huko, Prezzo ambaye jina lake halisi ni  Jackson Makini, alifichua kwamba mamake mzazi ni mzaliwa wa Mwanza na alikuwa akijihisi nyumbani.

Share This Article