Ruto: Kenya inaweza kufikia upeo wa ustawi duniani

Rais amesema ikiwa nchi zingine zilizostawi zaidi duniani zilifikia upeo huo, hakuna sababu ya Kenya kukosa kufuata mkondo huo. 

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto ameelezea imani yake kwamba Kenya inaweza ikabadilishwa na kuwa siyo tu nchi yenye kipato cha juu bali iliyostawi zaidi duniani.

Amesema kama nchi zingine zilizostawi zaidi duniani zilifikia upeo huo, hakuna sababu ya Kenya kukosa kufuata mkondo huo.

“Inawezekana, sisi tukiwa hai, tunaweza kufanya hilo. Kama wengine walifanya, nani alituroga sisi hatuwezi?” alishangaa Rais Ruto wakati akiwahutubia walinzi wa kibinafsi katika Ikulu ya Nairobi leo Alhamisi.

“Hata na sisi tunaweza Bwana! …Ndio hata wale wanajaribu kushindana na mimi nimewaambia wacheni ukabila, wacheni matusi, wacheni vitimbi, nyinyi mtueleze ajenda yenu ni gani? Sera yenu ni gani? Mpango yenu ni gani?”

Ili kuielekeza Kenya kujiunga na jumuiya ya mataifa yaliyostawi zaidi duniani, Ruto alisema utawala wake umezindua mipango kama vile nyumba za gharama nafuu, kubuni nafasi za ajira laki nane, nafasi za ajira za kidijitali laki tatu, na nafasi za ajira ughaibuni 580,000.

“Hao wanaojaribu kushindana na mimi, watatengeneza nafasi za ajira kutoka wapi?” Ruto aliurushia upinzani vijembe.

“Mambo ya hawa wapinzani wangu ni matatu – WANTAM, KASONGO, na MUST GO. Kwa hiyo mambo matatu, iko nafasi ya kazi hapo? Hawana mpango. Wale watu wako chini sana.”

 

 

Share This Article