Mwanamitandao maarufu kutoka Uganda, Tenge Tenge, anatarajiwa kufanya ziara yake ya kwanza jijini Kigali nchini Rwanda, ambapo atakuwa kivutio kikuu cha tamasha ya watoto iliyopatiwa jina la Tintin.
Tamasha hiyo itaandaliwa Jumamosi, Agosti 1, katika bustani ya Big Time iliyoko Kanombe, jijini Kigali nchini Rwanda.
Nyota huyo wa mitandaoni mwenye umri wa miaka 13, ambaye jina lake halisi ni Saad Ssozi, atatumbuiza pamoja na kundi la wacheza densi la Wembly Mo katika tamasha hiyo ya kifamilia inayotarajiwa kuvutia mamia ya watoto na wazazi.
Wasanii wengine wa Rwanda watakaoshiriki ni mtangazaji Uncle Banks, rapa Young Grace, Beyonce Cyuzuzo na DJ Crush.
Waandalizi walihamisha tamasha hiyo kutoka eneo la watoto kuchezea la Tintin huko Kimihurura hadi bustani ya Big Time kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.
Kabla ya tamasha, waandalizi wamezindua shindano la vipaji wakialika washiriki kupakia video zinazoonyesha uimbaji, uchezaji, uigizaji au kipaji kingine chochote kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia #TintinSummerFestival.
Mshindi atapata nafasi ya kutumbuiza jukwaani pamoja na Tenge Tenge wakati wa tamasha hilo.
Tenge Tenge alipata umaarufu duniani mwaka 2023 kupitia video zake za densi zilizosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuvutia nyota wa kimataifa kama Chris Brown, Davido, Tiwa Savage, Kai Cenat, IShowSpeed na Jason Derulo.