Rais wa Bangladesh Mohammed Shahabuddin, amejiuzulu kutokana na kile alichokitaja kuwa changamoto za kiafya.
Shahabuddin mwenye umri wa miaka 76, amejiuzulu baada ya kuhudumu miaka miwili, kwenye muhula wake wa miaka tano, hatua hiyo ikijiri wakati ambapo kumekuwa na shinikizo kutoka kwa upinzani kumtaka kuondoka mamlakani.
“Uchunguzi wa kimatibabu wa hivi karibuni umegundua naugua ugonjwa unaofahamika Autonomic Neuropathy. Kutokana na hali hiyo, mara kwa mara huwa napoteza ufahamu,” alisema Shahabuddin kupitia kwa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Mawasiliano.
Kulingana na taarifa hiyo, Spika wa Bunge la Taifa hilo atatekeleza majukumu ya Rais hadi Rais mpya atakapoteuliwa.
Rais mpya ni sharti ateuliwe ndani ya siku 90, kulingana na katiba ya taifa hilo.
“Ninaugua sana…. kwa hivyo sina uwezo wa kutekeleza majukumu yangu ya kikatiba,” aliongeza rais huyo kwenye barua aliyomwandikia spika wa Bunge la Taifa Hafiz Uddin Ahmed siku ya Ijumaa.
Spika wa Bunge Hafiz Uddin Ahmed, alikubali kujiuzulu kwa Rais huyo.