Mwanamuziki wa Kenya Nadia Mukami hii leo anatarajiwa kukutana na wafadhili wa tamasha yake ijayo ya kuadhimisha miaka 10 katika tasnia ya muziki.
Kupitia bango alilochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Nadia alisema mkutano huo unafanyika kati ya saa 12 jioni na saa tatu usiku katika hoteli ya Kingfisher, eneo la Westlands Nairobi.
“Tunaposherehekea miaka 10 ya Nadia Mukami, tuna furaha kuwaalika wafadhili wetu pamoja na washirika kwa mkutano wa dhifa ya wafadhili katika hoteli ya Kingfisher Hotels” aliandika Nadia.
Aliendelea kuelezea kwamba hafla hiyo ya kipekee inalenga kutoa shukrani kwa wote wanaounga mkono wazo lake la tamasha na kutembea naye katika safari yake katika muziki.
“Imani yenu isiyoyumba kwangu na kujitolea kwenu vimetekeleza jukumu muhimu katika kuafikia hatua hii,” alisema Nadia kwenye ujumbe wake akiongeza kwamba anatizamia jioni ya kipekee ya kutagusana na wanaoamini katika kazi yake.
Nadia Mukami anapanga kuandaa tamasha ya kuadhimisha miaka 10 ya kuwa mwanamuziki tarehe Mosi Agosti, 2026 katika eneo la burudani la Mass House, Nairobi.
Wasanii wanaotarajiwa kutumbuiza katika hafla hiyo ni pamoja na Nyota Ndogo, Sanaipei Tande, Maandy, Ssaru, Bahati, Dufla Diligon, Fena Gitu na wengine wengi.
Tangu alipoanza rasmi safari yake ya muziki, msanii huyo aliyeshinda tuzo mbalimbali amekua kutoka kuwa kipaji chipukizi hadi kuwa mmoja wa wanamuziki wa kike wanaotambulika zaidi Afrika Mashariki.