Wakenya wamemshambulia vikali mwigizaji wa Marekani Skai Jackson mitandaoni, kufuatia video yenye utata kuhusu ziara yake nchini.
Katika video hiyo, anadai kuwa vioo ni bidhaa ya gharama kubwa nchini ambayo Wakenya wengi hawawezi kumudu, akielezea kwamba watoto katika kijiji fulani waliona nyuso zao kwa mara ya kwanza kupitia simu yake ya mkononi.
Kauli hiyo imezua hasira kubwa kwenye mitandao ya kijamii, Wakenya wengi wakikosoa matamshi hayo wakisema yanaakisi mtazamo wa mwokozi na kuendeleza dhana potovu zilizochakaa kuhusu Afrika.
Utata huo ulianza baada ya Jackson kusimulia aliyoyapitia wakati wa ziara katika kijiji kimoja nchini Kenya, akiitaja kuwa ya kusikitisha lakini ya kufurahisha akidai kuwa vioo ni bidhaa adimu katika eneo hilo.
Aidha, alidai kuwa ukosefu wa vioo huenda unasaidia kupunguza hali ya watu kujihisi vibaya kuhusu muonekano wao na pia hupunguza unyanyasaji miongoni mwa vijana. Pia aliongeza kuwa, “Wanachukulia elimu kwa uzito mkubwa huko.”