Mashindano ya kitaifa ya kucheza densi yameanzishwa nchini Rwanda kwa mara ya kwanza kabisa, yakipatiwa jina la ‘Byina Rwanda’.
Pambano hilo litaandaliwa Agosti 15 hadi 17, 2026 katika Kituo cha Mundi mjini Kigali, yakiwa na lengo la kuhamasisha densi kama taaluma, kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa nchi hiyo na kutoa ajira kwa vijana.
Mashindano hayo, yaliyoandaliwa na RG Consult kwa ushirikiano na Kituo cha Taifa cha Utamaduni na Shirikisho la densi, yatawakutanisha wacheza densi kutoka maeneo mbalimbali nchini Rwanda, kuonyesha vipaji vyao katika densi za jadi, kisasa na za mitaani.
Kwa mujibu wa mratibu wa mashindano hayo, Remmy Lubega, mpango huo umeanzishwa ili kukabiliana na uhaba wa fursa kwa wacheza ngoma licha ya sekta hiyo kuendelea kukua kwa umaarufu na kuwa na mchango mkubwa kiuchumi.
Alisema mashindano hayo yanalenga kuifanya sekta ya densi kuwa ya kitaaluma kwa kuboresha viwango vya ubunifu wa miondoko, usimulizi wa hadithi, ubunifu wa mavazi na uzalishaji wa maonyesho, huku yakiiunga mkono sekta nzima ya ubunifu.
Wanaotaka kushiriki hawatalipa chochote ili kujisajili na usajili taendelea hadi Julai 22 kwa wacheza densi binafsi, wawili wawili na makundi, ambao wanatakiwa kujaza fomu ya maombi mtandaoni na kuwasilisha video ya maonyesho yao kwa ajili ya mchujo.
Mshindi wa jumla atajinyakulia zawadi ya fedha taslimu ya faranga milioni tano za Rwanda.
Waandaaji wanapanga kuanzisha mfumo wa upigaji kura wa umma ili kusaidia washiriki kugharamia maandalizi ya mashindano, huku wakitarajia kuyapanua.