Marekani inaitaka Iran itangaze hadharani kwamba Mlango wa Bahari wa Hormuz uko wazi na iahidi pia kusitisha mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara, kama sehemu ya mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika nchini Oman leo Jumamosi.
Vyombo vya habari vya Marekani viliwanukuu maafisa ambao hawakutajwa wakisema Tehran ilikuwa imewaeleza kwa faragha washauri wa Rais Donald Trump kuwa mashambulizi dhidi ya meli yalikuwa kosa.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa Iran ililaumu kundi moja la ndani lililojitenga kwa kuhusika na tukio hilo.
Trump amesema pande zote mbili zimekubaliana kuendelea na mazungumzo licha ya mapigano ya wiki hii kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambayo Ikulu ya White House iliona yalikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema nchi yake “imetimiza ahadi yake” kuhusu kusitisha mapigano, akisema kupitia mtandao wa X kwamba Marekani ndiyo ilikiuka makubaliano hayo.
Mwezi Juni, Marekani na Iran zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyoitaka Iran kuhakikisha meli za kibiashara zinapita salama.
Maafisa wakuu wa Marekani waliiambia wanahabari kwamba Tehran ilisema kundi “lililopotoka” la wenye msimamo mkali lilikuwa linajaribu kuhujumu mazungumzo kwa kushambulia meli za kibiashara.
Makamu wa Rais JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, pamoja na watu wawili ambao wamehusika kwa karibu katika mazungumzo ya Mashariki ya Kati—mjumbe maalum Steve Witkoff na mkwe wa Trump, Jared Kushner—wanatarajiwa kuongoza mazungumzo ya Jumamosi.