Mshambulizi wa Senegal, Sadio Mané, ametangaza kustaafu soka ya kimataifa kufuatia kubanduliwa kwa timu yake kwenye fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia na Ubelgiji katika raundi ya 16.
Mane, aliye na umri wa miaka 34 na anayechezea klabu ya Al Nassr, alitangaza kutundika daluga zake akihitimsiha amali yake ya soka ya kimataifa ya zaidi ya mwongo mmoja.
Ni mara ya pili kwa Mané kutangaza kustaafu soka ya kimataifa baada ya kusema hivyo punde baada ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mapema mwaka huu nchini Morocco.
Mané aliichezea Teranga Lions ya Senegal kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na kwa jumla alikuwa amesakata mechi zaidi ya 120 na kupachika magoli 52.
Aidha, Mané alitawazwa mwanandinga bora barani Afrika mara mbili.