Trump awasili nchini Uturuki kuhudhuria mkutano wa NATO

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais wa Marekani Donald Trump - Picha kwa hisani ya CNN

Rais wa Marekani Donald Trump amewasili nchini Uturuki na kulakiwa na mwenyeji wake Recep Tayyip Erdoğan. 

Trump ni miongoni mwa viongozi watakaohudhuria mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Kaskazini mwa Atlantiki, NATO ulioanza nchini Uturuki leo Jumanne.

Mkutano huo unaandaliwa katika mji mkuu wa Ankara na unatarajiwa kujadili masuala kama vile matumizi ya ulinzi, Ukraine na mivutano juu ya Iran.

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo uhusiano kati ya Marekani na NATO haujakuwa mzuri katika siku za hivi karibuni.

Trump amekuwa mstari wa mbele kuukosoa umoja huo kuhusiana na matumizi ya ulinzi, akizitaka nchi wanachama kutoa mchango zaidi wa fedha kwa umoja huo.

Mwezi jana, alimwambia Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte kuwa anataka uaminifu zaidi kutoka kwa umoja huo.

Rutte ameonekana kupinga shinikizo la Marekani akisema nchi  wanachama wa NATO zianaendelea kuziba pengo la matumizi.

Aidha, aliashiria kuwa nchi wanachama wa NATO zitatangaza makumi ya mabilioni ya dola katika mikataba mipya wakati wa mkutano huo wa siku mbili unaoanza leo Jumanne.

 

Share This Article