Carlo Ancelotti atasalia kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil maarufu kama Samba Boys hadi mwaka 2030, licha ya kubanduliwa katika raundi ya 16 ya Kombe la Dunia na Norway maajuzi.
Mkurugenzi Mkuu wa chama cha Soka nchini Brazil (CBF) Rodrigo Caetano amemtetea Ancelotti aliye na umri wa miaka 67, akisema kamwe hatapimwa kwa matokeo ya Kombe la Dunia mwaka huu pekee.
Mwitaliano huyo aliongeza mkataba wa kuendelea kusalia na Brazil mwezi Mei mwaka huu, kandarasi itakayodumu hadi mwaka 2030.
Ni miaka 28 tangu Brazil inyakue Kombe la Dunia kwa mara ya tano na walitimuliwa kwenye dimba la mwaka huu kufuatia kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Norway katika awamu ya 16 bora.