Kama njia moja ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa gharama nafuu, kampuni ya bima ya afya ya Jubilee imeanzisha kampeni ya kitaifa ya ‘Afya mtaani’ inayohamasisha umma kuhusu umuhimu wa kutafuta huduma bora za matibabu.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Jubilee Health Insurance Njeri Jomo, mpango huo utawezesha Wakenya kupata matibabu katika hospitali yoyote kwa gharama nafuu.
Chini ya kampeni hiyo, maafisa kutoka kampuni ya bima ya afya ya Jubilee watatembelea nyumba hadi nyumba kutoa ushauri na uhamasisho kuhusu umuhimu wa bima za afya.
“Wakenya wengi hawana bima siyo kwa sababu hawathamini bima ya afya bali kwa sababu ya nadharia kuwa bima ni ghali. Tunalenga kubadilisha mtazamo jinsi Wakenya watapata bima ya matibabu nchini, “ameema Jomo.
Kampeni hya Afya Mtaani imeanzia Nairobi kabla ya kuenezwa hadi maeneo mengine nchini.
Mpango huo unalenga kupiga jeki ajenda ya serikali ya upatikanaji wa huduma bora za afya na nafuu kwa Wakenya wote katika vituo vya afya.