Rais William Ruto leo Jumatatu katika Ikulu ya Nairobi ametia saini kuwa sheria Mswada wa Ugavi wa Mapato kwa serikali za kaunti wa mwaka 2026.
Sheria hiyo inatenga shilingi bilioni 428 kama mgao sawa wa mapato yaliyokusanywa na serikali zote 47 za kaunti.
Hii inaashiria asilimia 20.9 ya mapato ya kitaifa yaliyoidhinishwa ambayo ni zaidi ya asilimia 15 yanayohitajika kikatiba.
“Sheria hiyo inagawa kwa usawa mapato miongoni mwa kaunti 47, kuambatana na mfumo wa ugavi chini ya sehemu ya 217 ya katiba ya Kenya,” alisema Rais Ruto.
Mfumo huo, kulingana na Rais, unahakikisha ugavi sawa unaozingatia idadi ya watu, kiwango cha umaskini na ukubwa wa kimaeneo.
“Mgao huo utaimarisha ugatuzi, kwa kutoa rasilimali zinazohitajika ili kaunti zitekeleze wajibu wa kikatiba na utoaji huduma za ubora wa hali ya juu kulingana na bajeti na vipaumbele vya maendeleo,” aliongeza kiongozi wa taifa.