Canada yawatimua Afrika Kusini Kombe la Dunia

Canada wanasubiri mshindi wa mchuano wa Jumanne baina ya Morocco na Uholanzi katika raundi ya 16 bora Jumamosi hii.

Dismas Otuke
1 Min Read

Wenyeji wenza wa Kombe la Dunia  Canada ndio timu ya kwanza kufuzu kwa raundi ya 16 baada ya kuwatimua wawakilishi wa Afrika, Afrika Kusini bao moja kwa nunge katika mechi ya kwanza ya hatua ya 32 iliyoandaliwa Jumapili usiku uwanjani Los Angeles, Marekani.

Afrika Kusini ukipenda Bafana Bafana, waliokuwa na mashambulizi butu walikuwa wakijihami wakitarajia sare ili mechi iamuliwe kupitia dakika 30 za mazidadi, lakini Stephen Eustaquio alitibua njama yao akivurumisha kombora la dakika ya 92 kutoka nje ya kijisanduku kwa bao la ushindi.

Tobwe hilo la pembeni kushoto lilimpata hoi bin taaban Kipa Ronwen Williams wa Afrika Kusini huku mashabiki wa Canada wakisherehekea bao la ushindi.

Canada wanasubiri mshindi wa mchuano wa mapema Jumanne kati ya Morocco na Uholanzi.

Mechi tatu zaidi za awamu hiyo zitapigwa baina ya leo Jumatatu usiku na mapema Jumanne.

 

Share This Article