Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda amemtetea Rais William Ruto akisema kuwa anapaswa kupimwa kwa matokeo ya utendaji kazi wa serikali yake badala ya kukosolewa kwa ratiba yake ya kazi inayodaiwa kuwa yenye shughuli nyingi.
Kupitia taarifa aliyochapisha kwenye mitandao yake ya kijamii, Jhanda alisema uongozi hupimwa kwa utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi, wala si kwa mitazamo kuhusu namna rais anavyosimamia shughuli za serikali.
“Uongozi hupimwa kwa matokeo, si kwa jinsi wakosoaji wanavyodhihaki ratiba yenye shughuli nyingi,” alisema Jhanda.
Mbunge huyo alipuuza madai kwamba mtindo wa Rais Ruto wa kufuatilia kwa karibu shughuli za serikali ni ishara ya kutaka kudhibiti kila jambo, akisisitiza kuwa usimamizi wa karibu ni ishara ya uwajibikaji si udikteta.
“Wale ambao hawakuwahi kudhani William Ruto angeendelea kuwa na maadili makubwa ya kazi sasa wanaita kujituma huko kuwa ni ‘udhibiti’,” aliandika kwenye mtandao wake wa X.
Jhanda alisisitiza kuwa ni jukumu la Rais kusimamia utekelezaji wa mipango ya serikali na kuhakikisha wizara pamoja na taasisi za umma zinatimiza wajibu wao.
“Usimamizi si utawala wa kiimla. Uwajibikaji si udikteta,” alisema.
Aidha, alielezea kuwa kila serikali inapaswa kutathminiwa kwa kuzingatia sera zake, mafanikio yake na kuheshimu taasisi za kidemokrasia, badala ya kuangalia idadi ya saa ambazo rais hufanya kazi.
Kauli za Jhanda zinajiri wakati mjadala ukiendelea kuhusu mtindo wa uongozi wa Rais Ruto, huku wafuasi wake wakisifu ushiriki wake wa karibu katika utekelezaji wa miradi ya serikali na kufanya maamuzi, ilhali wakosoaji wakidai kuwa kugawa majukumu zaidi kungesaidia kuimarisha utawala.
Matamshi hayo yanatarajiwa kuongeza mjadala wa kitaifa kuhusu uongozi wa mamlaka ya utendaji huku serikali ya Kenya Kwanza ikiendelea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo chini ya uangalizi mkali wa kisiasa.