Serikali yawakaribisha watalii, yawahakikishia hakuna maambukizi ya Ebola

Bitok alisema serikali imeweka mikakati madhubuti ya kutambua mapema, kudhibiti na kushughulikia kisa chochote kinachoshukiwa kuwa cha ugonjwa huo

Tom Mathinji
2 Min Read
Julius Bitok - Katibu katika Wizara ya Utalii .

Serikali imewahakikishia Wakenya na watalii kwamba taifa hili limejitayarisha vilivyo kukabiliana na dharuta yoyote ya Ebola, ikisema hakuna kisa cha ugonjwa huo kimeripotiwa nchini.

Hakikisho hilo limetolewa na Katibu katika Wizara ya Utalii Prof. Julius Bitok aliyezungumza katika mkutano wa Chama cha Wamiliki, Wahudumu wa Hoteli na Wapishi (KAHC) mjini Malindi, kaunti ya Kilifi.

Ametaja kuwa za kupotosha ripoti zinazoashiria kwamba Kenya inakabiliwa na ugonjwa wa Ebola akiongeza kuwa hatua zinazotekelezwa na serikali ni za kujihadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Kulingana na Prof. Bitok, serikali imeweka mikakati madhubuti ya kutambua mapema, kudhibiti na kushughulikia kisa chochote kinachoshukiwa kuwa cha ugonjwa wa Ebola.

Amewahimiza watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani kutofuta mipango yao ya kusafiri nchini, akisisitiza kuwa Kenya iko wazi, ni salama, na iko tayari kuwakaribisha wageni wote.

“Nawahakikisha Wakenya na raia wa kigeni kuwa Kenya ni salama.  Hakuna maambukizi ya Ebola hapa nchini. Serikali imeweka mikakati thabiti ya kutambua, kudhibiti na kushughulia kisa chochote kinachoshukiwa. Tunawahimiza watalii kuzuru Kenya. Kenya iko wazi, salama na tayari kuwakaribisha,” alisema Katibu huyo aliyejiunga na wizara hiyo siku chache zilizopita.

Prof. Bitok, ambaye awali alihudumu kama Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi, alisema Kenya kwa sasa hupokea watalii milioni 1.5 kila mwaka, idadi aliyoitaja kuwa ya chini ikilinganishwa na uwezo wa utalii wa taifa hilo.

Ni kwa misingi hiyo ambapo ametoa wito kwa asasi za serikali zinazohusika na kupigia debe utalii nchini Kenya kuimarisha juhudi zao ili kuwezesha taifa hili kuwavutia watalii milioni tano kufikia mwezi Disemba mwaka huu.

Share This Article