Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetangaza matibabu bila malipo kwa magonjwa yote katika eneo la Ituri, huku taifa hilo likiendelea kukabiliana na chamko la ugonjwa wa Ebola.
Maambukizi ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC yameongezeka, na sasa zaidi ya visa 1000 vimethibitishwa.
Waziri wa Afya wa DRC Samuel Roger Kamba amesema hatua hiyo inatekelezwa katika mkoa wa Ituri ambako ugonjwa huo ulizuka.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauathiri dharura zingine za kiafya nchini DRC,” alisema Kamba.
Amesema mpango huo wa majaribio wa Ituri unajumuisha kupata maelezo ya afya bila malipo na matibabu ya magonjwa yote.
Aidha, ameongeza kuwa mpango huo utafadhiliwa na ushuru wa afya ulioanzishwa mwezi Machi pamoja na bima ya afya ya lazima.