Keir Starmer atangaza kujiuzulu kama Waziri Mkuu wa Uingereza

Starmer aliingia madarakani kama Waziri Mkuu wa Uingereza mwezi Julai mwaka 2024.

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri Mkuu wa Uingereza anayeondoka, Keir Stamer / Picha kwa hisani ya PA Media

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ametangaza kuwa atajiuzulu kutoka kwenye wadhifa huo.   

Amesema imekuwa fahari yake kuhudumu kwenye wadhifa huo tangu alipoingia madarakani mwezi Julai mwaka 2024.

Starmer amesema tayari amemuarifu Mfalme Charles III wa nchi hiyo kuhusu hatua yake ya kujiuzulu.

“Nitajiuzulu kama kiongozi wa chama cha Labour,” pia alitangaza Starmer aliyeandamana na mkewe wakati akitangaza hayo nje ya ofisi ya Waziri Mkuu iliyo kwenye barabara ya Downing Street.

Akitangaza hatua ya kuachia ngazi leo Jumatatu, Starmer ameitaka Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama cha Labour kuandaa ratiba ya kumtafuta mrithi wake huku mchakato wa uteuzi  ukipangwa kufanyika Julai 9 na kuhitimishwa kufikia wakati bunge litaenda mapumzikoni wakati wa msimu wa joto.

Hii ina maana kwamba nchi hiyo itakuwa na Waziri Mkuu mpya kabla ya bunge kurejelea vikao vyake mwezi Septemba mwaka huu.

Wakati wa kipindi hicho cha mpito, Starmer ataendelea kuhudumu kama Waziri Mkuu.

Starmer alichukua wadhifa huo kutoka kwa Rishi Sunak aliyehudumu kama Waziri Mkuu wa Uingereza kati ya mwaka 2022 na 2024.

 

Share This Article