Shule ya wasichana ya State House yafungwa kwa muda

Wanafunzi wameteketeza au kuharibu mali ya shule kadhaa humu nchini tangu mwishoni mwa mwezi jana.

Dismas Otuke
1 Min Read

Shule ya upili ya wasichana ya State House imefungwa kwa muda usiojulikana huku wazazi wakiwachukua watoto wao.

Mwalimu Mwandamizi wa shule hiyo Josephine Mwongera, aliwaarifu wazazi wafike shuleni mapema leo, Juni 9 kuwachukua wanafunzi.

Mwongera alisema sababu ya kufungwa kwa shule kulitokana na hatua ya wanafunzi kutishia kuzua rabsha ikichangiwa na misukosuko na ukosefu wa utulivu wa wanafunzi unaoshuhudiwa katika shule nyingi nchini.

Wanafunzi wameteketeza au kuharibu mali ya shule kadhaa humu nchini tangu mwishoni mwa mwezi jana.

Ni hatua ambayo imezifanya shule nyingi kuchukua tahadhari kabla ya maji kuzidi unga kama ilivyoshuhudiwa katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru.

Kwenye mkasa wa moto uliotokea shuleni hapo, wanafunzi 16 walifariki kwenye mkasa wa moto huku wengine 79 wakijeruhiwa.

Angalau wanafunzi 9 wanazuiliwa kwa madai ya kuwasha moto huo ulioteketeza bweni usiku wa manane mwishoni mwa mwezi jana na pia kusababisha uharibifu mkubwa.

Share This Article