Rais William Ruto amesema mipango kabambe imewekwa na utawala wake kwa lengo la kujenga mabwawa makubwa 50 kote nchini.
Serikali pia itajenga mabwa ya kati na madogo 200 na maelfu ya mabwawa mengine madogo zaidi kote nchini.
Ruto amesema ujenzi wa mabwawa hayo utaongeza idadi ya ekari kunakofanywa kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji hadi milioni 2.5 kati ya kipindi cha miaka mitano hadi saba ijayo.
Mabwawa hayo, mengi ambayo yatajengwa kaskazini mwa nchi, yanajumuisha bwawa la Isiolo kwenye mto Ewaso Nyiro, The High Grand Falls Dam kwenye Mto Tana na Bwawa la Bute huko Wajir Kasakazini miongoni mwa mengine.
“Kila ya mabwawa haya ni dhihirisho kwamba hakuna kaunti ambayo iko mbali zaidi kiasi cha kutopata maendeleo, na hakuma mto uko mbali zaidi kiasi cha kutoweza kutumiwa kwa manufaa ya Kenya,” alisema Rais Ruto wakati wa sherehe za Sikukuu ya Madaraka.