Rais Ruto kufanya ziara rasmi Afrika Kusini

Ziara hiyo rasmi itajumuisha sherehe ya makaribisho, na kufuatiwa na mazungumzo ya pande mbili kati ya viongozi hao wawili na kisha mkutano wa kibiashara utakaowajumuisha maafisa wa serikali na wale wa sekta ya kibinafsi kutoka nchi hizo mbili.

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

Rais William Ruto anatarajiwa kufanya ziara rasmi ya siku tatu nchini Afrika Kusini juma lijalo kwa mwaliko wa Rais Cyril Ramaphosa.

Kwenye ukurasa wake wa X, Rais Ramapohosa alisema amemwalika kiongozi huyo wa Kenya kuanzia Juni 3 hadi Juni 5, 2026.

“Rais Ruto atafanya ziara ya kiserikali kuanzia Juni 3 hadi 5 kwa mwaliko wa Rais Ramaphosa. Afrika Kusini inadhamini Kenya kama mshirika wa kimkakati katika kanda ya Afrika Mashariki na katika bara hili,” alisema Ramaphosa alipokuwa akitoa ratiba ya ziara hiyo.

Afrika Kusini na Kenya zimefurahia ushirikiano wa muda mrefu ambao ni wa manufaa kwa pande mbili tangu uhusiano wa kidiplomasia kubuniwa upya mwaka 1994.

Ziara hiyo rasmi itajumuisha sherehe ya makaribisho, na kufuatiwa na mazungumzo ya pande mbili kati ya viongozi hao wawili na kisha mkutano wa kibiashara utakaowajumuisha maafisa wa serikali na wale wa sekta ya kibinafsi kutoka nchi hizo mbili.

Mkutano huo wa kibiashara utalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kubuni mikakati ya kupanua fursa za kibiashara na uwekezaji katika sekta muhimu kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

Share This Article