Makamu wa Rais wa Marekani, J.D. Vance amesema kuwa Marekani na Iran bado zinapaswa kutatua masuala kadhaa yaliyosalia kabla ya kufikiwa kwa makubaliano kuhusu vita.
Akijibu swali la BBC kuhusu iwapo Rais wa Marekani, Donald Trump, yuko karibu kutia saini makubaliano hayo, Vance amesema bado ni mapema kueleza “lini au kama” pande hizo mbili zitafikia makubaliano ya mwisho.
Makubaliano hayo yanadaiwa kujumuisha kuongezwa kwa muda wa kusitisha mapigano kwa siku 60 pamoja na kuanza kwa mazungumzo kuhusu mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran.
Mapema Alhamisi, maafisa wa Marekani waliiambia BBC kwamba mataifa hayo mawili yalikuwa yamefikia mwafaka kuhusu mfumo wa makubaliano hayo, lakini yakahitaji kwanza kuidhinishwa na Donald Trump pamoja na viongozi wa Iran.
Hata hivyo, shirika la habari la Tasnim ambalo lina uhusiano wa karibu na serikali ya Iran, liliripoti kuwa makubaliano hayo bado hayajakamilishwa wala kuthibitishwa rasmi.
Vance alisema Alhamisi jioni kuwa wapatanishi kutoka pande zote mbili walikuwa bado “wakijadiliana kwa kina kuhusu masuala kadhaa yanayohusu maandishi ya makubaliano,” likiwemo “suala la urutubishaji.”
“Bado hatujafikia hitimisho la mwisho, lakini tuko karibu sana na tutaendelea kulifanyia kazi,” aliwaambia waandishi wa habari.
Taarifa ya BBC