Rais William Ruto ametuma risala za rambirambi kwa familia za wanafunzi walioangamia kutokana na mkasa wa moto katika shule ya Utumishi Girls Academy, mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru.
Jumla ya wanafunzi 16 waliangamia kwenye msaka huo uliotokea usiku wa manane huku saba kati ya wanafunzi 79 waliojeruhiwa wakiwa bado wamelazwa hospitalini.
“Mioyo na maombi yetu ni kwa familia zilizopoteza binti zao wapendwa katika mkasa wa moto katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil. Hakuna maneno yanaweza yakafuta uchungu wa kumpoteza mtoto mdogo aliyekuwa na ahadi, matumaini, na ndoto za siku zijazo,” alisema Rais Ruto kwenye risala yake.
“Kama taifa, tunaomboleza na wazazi, walezi, walimu na wanafunzi wanaostahimili mkasa huu.”
Rais amesema kwa sasa, juhudi zote zinaelekezwa kwa uokozi wa wale wote walioathiriwa, matibabu ya waliojeruhiwa na kuzisaidia familia zao.