Kenya na Angola zimetia saini makubaliano ya ushirikiano wa Ulinzi, katika hafla iliyoandaliwa kwenye Makao Makuu ya Ulinzi Jijini Nairobi.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya na mwenzake wa Angola Jenerali Mstaafu Lúcio Gonçalves Amaral.
Kulingana na Tuya, makubaliano hayo yanaashiria hatua kubwa katika kuimarisha ushirikiano wa pamoja katika kuboresha udumishaji amani, usalama na uthabiti wa kikanda.
“Makubaliano hayo yatabuni mikakati ya ushirikiano,na utoaji mafunzo miongoni mwa maswala yaliyoafikiwa,” alisema Waziri Tuya.
Wengine walioshuhudia hafla hiyo ni pamoja na balozi wa Angola nchini Kenya Mario Azevedo Constantino, Naibu Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya anayehusika na maswala ya operesheni na mafunzo (ACDF OPD&T), Meja Jenerali Fredrick Leuria, na maafisa wengine wakuu wa kijeshi kutoka Kenya na Angola.