Kindiki: Serikali imepiga hatua kubwa kuimarisha sekta ya elimu

Kindiki alisema bajeti ya sekta ya elimu iliongezwa kutoka shilingi bilioni 500 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 702 katika bajeti ya sasa.

Tom Mathinji
2 Min Read
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki katika shule ya Geturi kaunti ya Kisii.

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, ameelezea hatua zilizopigwa na serikali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini Kenya.

Akizungumza Jumatatu baada ya kuzindua shule ya Geturi katika eneo la Mosocho, eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini, kaunti ya Kisii, Naibu huyo wa Rais alisema utawala wa Kenya Kwanza umeongeza ufadhili katika sekta ya elimu kama sehemu ya mpango wake wa kufanikisha upatikanaji wa elimu, na kuimarisha viwango vya ubora kote nchini.

Kindiki alisema bajeti ya sekta ya elimu iliongezwa kutoka shilingi bilioni 500 mwaka 2022 hadi shilingi bilioni 702 katika bajeti ya sasa, na itaongezeka hadi shilingi bilioni 765 katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2026/2027.

Wakati huo huo, Kindiki alisema serikali imetekeleza sera kadhaa ikiwa ni pamoja na Mafunzo ya Elimu ya umuilisi (CBET), uajiri wa walimu, na upanuzi wa miundombinu ya elimu.

“Tunawekeza zaidi katika sekta ya elimu kwa sababu ndio msingi thabiti na iliyo na fursa ya mabadiliko ya kitaifa,” alisema kindiki.

Alidokeza kuwa serikali imewaajiri walimu 100,000 katika muda wa miaka minne iliyopita, ujenzi wa madarasa 23,000 na maabara 1,600 ili kuboresha elimu kote nchini.

Aidha, aliahidi kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, uajiri wa walimu na kupiga jeki mipango ya wanafunzi kuhakikisha kila mwanafunzi anaopata elimu bora.

Share This Article