Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa serikali kutafuta kila mbinu ya kuwakinga Wakenya dhidi ya bei za juu za mafuta.
Aidha, ameashiria kuwa yuko tayari kusaidia kuangazia suala hilo ikiwa msaada wake utatafutwa.
“Watu wanapiga kelele kwa sababu wanasema jamani, mimi ni mtu ambaye mshahara wangu ni shilingi elfu 20, hiyo elfu 20, 800 inaenda kwa petroli pekee yake, kwa matatu kwenda na kurudi nyumbani, elfu 12 inaenda kwa nyumba ambayo nimekodisha, nimebaki na elfu 2 ya kulisha watoto wangu na kuwapeleka shule. Hiyo ndio shida, ongelesha shida,” alisema Uhuru wakati akiwahutubia wajumbe wa chama cha Jubilee katika kaunti ya Kiambu leo Jumatatu.
“Hapana ongea mambo ya kabila na ya nini. Na kama unataka tusaidiane kutatua hiyo shida semeni, tutatue hiyo.”
Rais huyo wa zamani aliyasema hayo siku chache baada ya Rais William Ruto kukutana na wadau wa sekta ya uchukuzi wa umma katika Ikulu ya Mombasa Ijumaa wiki iliyopita.
Wakati wa mkutano huo, Rais Ruto alitangaza kuwa bei ya dizeli itapunguzwa kwa shilingi 10 zaidi wakati bei mpya za mafuta zitakapotangazwa mwezi ujao kwa kipindi cha kati ya Juni 15 na Julai 14.
Bei hizo hutangazwa na Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli, EPRA tarehe 14 ya kila mwezi.
“Nimeagiza kwamba katika kipindi kijacho cha kutangaza bei mpya za mafuta, serikali itapunguza bei ya dizeli kwa shilingi 10 zaidi kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Julai,” alisema Rais Ruto wakati akihutubia taifa siku hiyo.
“Hatua hii inalenga kudhibiti bei za mafuta na kutoa afueni zaidi kwa watumiaji.”