Shirika la Reli la Kenya (KR) lile la Uganda (URC) zimeimarisha ushirikiano wao katika uchukuzi wa mizigo na abiria kati ya Kenya na Uganda.
Majadiliano hayo yaliandaliwa kati ya bodi ya usimamizi ya Shirika la Reli la Kenya na bodi mpya ya usimamizi wa reli nchini Uganda ambayo ilikuwa kwenye ziara ya kujifahamisha kati ya Bandari ya Mombasa na Uganda.
Ujumbe huo wa Uganda uliongozwa na mwenyekiti wa bodi ya URC Daudi Migereko, huku upande wa Kenya uliongozwa na mwenyekiti wa bodi ya KR, Abdi Bare Duale na Mkurugenzi Mkuu Philip Mainga.
Mazungumzo ya pande hizo yaliangazia kuimarisha uunganishaji, kuboresha ushughulikiaji wa mizigo, na kuweka usafiri wa reli kuwa wenye ushindani katika uchukuzi wa mizigo Afrika Mashariki.
Kulingana na mwenyekiti wa Shirika la Reli la Kenya, Abdi Bare Duale alihakikisha kujitolea kwa Shirika hilo kufanikisha uchukuzi wa mizigo zinazoelekea Uganda kutoka Bandari ya Mombasa.
Aidha, alidokeza kuwa KR itabuni uwezo wa uchukuzi wa kibiashara, ili kupiga jeki ukuaji wa biashara na utangamano wa kiuchumi.