EPRA yapunguza bei ya dizeli, yaongeza bei ya mafuta taa

Hata hivyo, wahudumu wa uchukuzi wa umma wanashikilia kuwa mgomo wa matatu utaendelea hadi serikali ipunguze bei ya mafuta kwa hadi shilingi 30-35.

Tom Mathinji
2 Min Read
EPRA yapunguza bei ya diesel, yapandisha bei ya mafuta taa.

Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli nchini Kenya (EPRA), imepunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shilingi 10.06 kwa lita huku ikiongeza bei ya mafuta taa kwa shilingi 38.60 kwa kila lita.

Kupitia kwa taarifa jana Jumatatu jioni, EPRA ilisema bei hizo mpya zitatekelezwa kuanzia leo Jumanne, Mei 19, 2026 hadi Juni 14, 2026.

Kufuatia mabadiliko hayo, lita moja ya mafuta ya super petrol jijini Nairobi itauzwa kwa shilingi 214.25, dizeli shilingi 232.86 na mafuta taa shilingi 191.38.

Hatua ya EPRA inafuatia malalamishi kutoka kwa wahudumu katika sekta ya uchukuzi wa umma, ambao waliandaa mgomo wa kitaifa ulioanza jana Jumatatu na kusambaratisha shughuli za uchukuzi kote nchini.

Wasafiri walitatizika na kulazimika kusalia nyumbani baada ya kukosa usafiri, huku wahudumu wa uchukuzi wa umma wakishikilia kuwa wataendelea na mgomo huo hadi bei ya mafuta ipunguzwe zaidi.

Huku wahudumu wakitaka bei ya mafuta kupunguzwa kwa shilingi 46, serikali inasema inaweza tu kupunguza bei hiyo kwa shilingi 10.

Ni hali iliyosababisha pande hizo mbili kutofikia makubaliano hiyo jana na wahudumu wa uchukuzi wa umma kutangaza kuwa mgomo wao utaendelea hadi makubaliano na serikali yafikiwe.

Kulingana na Wizara ya Usalama wa Taifa, watu wanne walifariki kutokana na maandamano yaliyoshuhudiwa kote nchini hiyo jana, kulalamikia bei ya juu ya mafuta.

 

TAGGED:
Share This Article