Uganda na Ivory Coast zilianza fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 17, kwa ushindi Jumatano, huku wenyeji na mabingwa watetezi Morocco, wakiambulia sare .
Morocco walitoka nyuma na kulazimisha sare ya bao moja dhidi ya Tunisia, katika kundi A,huku Misri na Ethiopia, wakitoka sare tasa katika pambano jingine kundini humo.
Katika kundi B,Ivory Coast, iliwanyuka Cameroon 2-0, wakati Uganda, ikiwalaza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo magoli 3-0.
Mechi nne zitachezwa Alhamisi,Mali wakipambana na Angola, kundini C saa kumi, huku majirani Tanzania na Msumbiji, wakitoana jasho saa moja usiku.
Senegal watachuana na Afrika Kusini, saa moja usiku katika kundi D, wakati Algeria wakimaliza udhia na Ghana saa nne usiku.
Fainali ya kipute hicho itasakatwa Juni 2, huku timu 10 bora zikifuzu kwa Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Qatar.