Mwimbaji wa nyimbo za injili wa asili ya Uganda Julie Birungi amesema kwamba anahisi ametengwa na waimbaji wenza.
Hii ni baada yao kukosa kuhudhuria tamasha aliyoandaa kwenye siku ya kina mama ulimwenguni.
Msanii huyo alikuwa ameandaa tamasha hiyo huko Toronto, na anaamini kutohudhuriwa kwake kunatokana na ubaguzi kwa misingi ya maisha yake binafsi.
Akizungumza baada ya tamasha hiyo aliyoipa jina la “An Evening with Julie”, Birungi alisema ameumia baada ya orodha nzima ya wasanii waalikwa kutofika siku ya tukio hilo.
Mwimbaji huyo alilazimika kutumbuiza pamoja na watoto wake, Ezekiel na Esther pekee.
“Mnaweza kuwa mnajiuliza kwa nini wasanii hawa hawapo hapa leo, ni kwa sababu mimi ni tofauti kwa namna wanavyoona kuwa mimi ni tofauti,” alielezea Birungi.
Usemi wake huenda unarejelea hali yake ya kuwa katika ndoa ya jinsia moja, baada ya kutengana na aliyekuwa mume wake na baba ya watoto wake.
“Hawa ni watu niliowaita marafiki zangu. Tulikuwa tukicheka pamoja, kulia pamoja, kufanya utani na kusimamana. Lakini kumbe nilikuwa nimekosea,” aliongeza.
Mama huyo anasema kwamba hakuwahi kuhitaji waimbaji hao awali, “Lakini moyoni nilijua nina marafiki wa kukimbilia nitakapowahitaji. Nafikiri nilikuwa nimekosea.”
Birungi alifichua kuwa baadhi ya wasanii hao mwanzoni walitoa visingizio vya kutohudhuria, lakini baadaye wakaacha kabisa kujibu simu au ujumbe wake. Anaamini kuwa kujiondoa kwao hakukuwa bahati mbaya, bali kulihusiana na jinsi wanavyomtazama.
“Mnataka kunipenda kwa siri. Nimeshindwa kuelewa. Mnatakiwa kuonyesha upendo, kusambaza upendo, lakini mnabagua watu kama mimi,” alisema.
Alishangaa watu kama yeye wanapaswa kwenda wapi, akiongeza kuwa wasanii hao walikuwa wamethibitisha mapema kuwa wangehudhuria, lakini wakajiondoa dakika za mwisho, jambo analoamini lilitokana na kutoridhishwa kwao na mwelekeo wake wa ndoa.
Kwa mujibu wa Birungi, maandalizi ya tamasha hiyo yalianza mwaka jana, na yeye binafsi aliwasiliana na wasanii wote aliotarajia kushiriki katika tukio hilo, akiwemo Judith Babirye, Vivian Tendo, Jackie Ssenyonjo na Mr Samuel, miongoni mwa wengine.
Julie Birungi, ambaye zamani alijulikana kama Julie Mutesasira, ni mke wa zamani wa mchungaji, alihamia Canada, ambako baadaye alijitokeza hadharani kuhusu mwelekeo wake wa mahusiano na kuolewa tena.