Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema kwamba atasalia madarakani licha ya Mahakama ya Katiba Nchini humo kufufua upya mchakato wa kumuondoa madarakani.
Mchakato huo ulitokana na tuhuma za kiongozi huyo kuficha tukio la wizi lililotokea mwaka 2020 kwenye makazi yake ya shamba la Phala Phala.
Ramaphosa alitoa kauli hiyo kupitia hotuba ya televisheni jana usiku Mei 11, 2026 baada ya kufanya vikao na Washauri wake wa kisiasa na kisheria.
Alihusisha pia maafisa waandamizi wa afisi ya Rais, ambapo amesisitiza kuwa hakuna uamuzi wa mahakama unaomlazimisha kuachia madaraka yake kwa sasa.
Mahakama hiyo imefufua mchakato huo baada ya ripoti ya jopo huru lililoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Sandile Ngcobo kubaini kuwa huenda Ramaphosa alikiuka misingi ya ofisi yake na kuingia katika mgongano wa maslahi kati ya wajibu wake wa umma na shughuli zake binafsi.
Hata hivyo, Ramaphosa amesema ripoti hiyo ina mapungufu makubwa na ametangaza kuwa ataomba mahakama kuu kudurusu ripoti hiyo.
“Nimeendelea kusisitiza kuwa sijawahi kuiba fedha za umma, kufanya uhalifu wowote wala kukiuka kiapo changu cha uongozi, sitajiuzulu kwa sababu kufanya hivyo kutakuwa ni kuhukumu mchakato wa Kikatiba kabla haujakamilika na kutoa uzito kwa ripoti ambayo ina kasoro kubwa,” amesema Ramaphosa.