Usalama umeimarishwa katika jiji la Nairobi huku kongamano la Africa Forward likianza leo kwa kuwasili kwa wajumbe.
Kamanda wa polisi katika eneo la Nairobi Issa Mohammud alihakikishia umma kwamba maafisa wa usalama wametumwa kushika doria katika maeneo yote yatakayotumika wakati wa hafla hiyo.
Huku hayo yakijiri, shughuli za uchukuzi zinatarajiwa kutatizwa pakubwa jijini Nairobi kuanzia leo hadi Jumanne, wakati wa kongamano la ustawi wa bara Afrika.
Kesho Jumatatu na Jumanne, barabara za katikati mwa jiji la Nairobi za City Hall, Parliament, Harambee Avenue na Taifa Road zitafungwa kwa umma kwa ajili ya matumizi ya magari yatakayokuwa yakielekea kwenye ukumbi wa KICC pekee.
Mohamud alitoa wito kwa waendeshaji magari kuwa watulivu, kuzingatia kanuni za barabarani na kufuata maagizo ya maafisa wa trafiki watakaokuwa katika maeneo yatakayoathiriwa.
Awali Rais William Ruto, Waziri aliye na mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Musalia Mudavadi na mwenzake wa utalii Rebbeca Miano walithibitisha kukamilika kwa maandalizi kwa ajili ya kongamano hilo.
Linaandaliwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Kenya na ile ya Ufaransa na ndio mara ya kwanza linaandaliwa katika taifa ambalo halitumii lugha ya kifaransa.