Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi, amesema mkutano wa Africa Forward 2026 utakaoandaliwa Nairobi juma lijalo, utaangazia kutoa kursa za uwekezaji, kubuni nafasi za ajira na kuiweka Afrika katika nafasi nzuri ya kuchochea mabadiliko ya kiuchumi duniani.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuikabidhi rasmi Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC) ambalo litaandaa mkutano huo, Mudavadi alidokeza kuwa Kenya inatarajia kuwa mkutano huo utatoa suluhu ambazo zitawafaidi raia wa Afrika moja kwa moja.
Mkutano huo utaandaliwa Jijini Nairobi Mei 11 na 12, na utahudhuriwa na zaidi ya Marais na viongozi 30 wa nchi na serikali, huku zaidi ya wajumbe 4,000, wafanyabiashara, wawekezaji na washirika wa maendeleo wa Afrika, Ufaransa na kote duniani pia wakitarajiwa kwenye kongamano hilo.
“Tunalenga kuleta matokeo ambayo yatasababisha kubuniwa kwa nafasi za ajira, kuimarisha ukuaji wa viwanda na mustakabali bora kwa wananchi wetu,” alisema Mudavadi.
Mudavadi ambaye pia ni Mkuu wa Mawaziri, alitaja mkutano huo kuwa wa kwanza kuandaliwa katika taifa lisilozungumza lugha ya Kifaransa barani Afrika.
“Huu utakuwa mkutano wa kwanza kuandaliwa katika taifa lisilozungumza lugha ya Kifaransa Afrika, hatua inayoashiria kuimarika zaidi kwa uhusiano wa Afrika na Ufaransa.