Rais wa Kenya William Ruto, amewahakikishia wakazi wa kaunti ya Laikipia kuwa maafisa wa usalama wataakabiliana vilivyo na majangili ambao wamejificha kwenye msitu wa Mukogodo.
Msitu huo unapatikana Kaskazini Mashariki mwa Laikipia karibu na mpaka wa Isiolo.
Akizungumza akiwa Doldol, kaunti ndogo ya Laikipia Kaskazini, Ruto alionya kuwa chuma cha majangili hao ki motoni, huku akiwahimiza kujisalimisha kabla ya kufikiwa na mkono mrefu wa serikali.
Kiongozi huyo wa taifa, alidokeza kuwa utawala wake umemakinika kupeleka maendeleo katika pembe zote za Kenya bila ubaguzi.
Miongoni mwa miradi ambayo serikali kuu itatekeleza katika kaunti ya Laikipia ni pamoja na ujenzi wa kilomita 60 za barabara kutoka Nanyuki hadi Doldol, na kilomita zingine 216 za barabara katika kaunti nzima ya Laikipia.
Rais Ruto alikuwa ameandamana na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, mbunge wa Laikipia Kaskazini Sarah Korere, aliyekuwa spika wa Bunge la Taifa Francis Ole Kaparo, na mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) Ndiritu Muriithi miongoni mwa wengine.