Karua afika Kampala kumwakilisha Besigye mahakamani

besigye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini na umiliki haramu wa silaha, akituhumiwa na serikali ya Uganda kwa kupanga njama za kuipindua serikali.

Marion Bosire
2 Min Read

Wakili Mkuu wa Kenya Martha Karua jana alikuwa jijini Kampala, nchini Uganda kwa ajili ya kumwakilisha kiongozi wa upinzani nchini humo Dkt. Kizza Besigye.

Karua aliyewahi kuhudumu kama waziri wa masuala ya haki nchini Kenya, alichapisha picha iliyomwonyesha yeye na wenzake wakiwa nje ya mahakama kuu ya Kampala.

Katika chapisho hilo, wakili huyo alimshangaa Besigye aliyekamatwa na kuwekwa rumande kwa zaidi ya siku 500, afya ikadhoofika na bado anaweza kutembea mwenyewe kuingia mahakamani akiwa na msimamo ule ule.

“Inakukumbusha kwamba heshima ni upinzani wa aina yake,” Alisema Karua akiongeza kuelezea kwamba alikuwa amerejea Kampala jana kama mmoja wa wanasheria wanaomwakilisha Besigye.

Martha ambaye pia ni kiongozi wa chama cha PLP alisema kwamba tangu mwanzo, kesi hiyo imekuwa ikigubikwa na vitendo vya ukiukwaji wa sheria, ucheleweshaji wa makusudi na ukiukaji wa kimfumo wa taratibu za haki.

“Azimio letu la kusimama dhidi ya hayo halijayumba kamwe.Jumuiya yetu inaendelea kukabiliwa na vitisho vya kudhoofishwa kwa demokrasia, lakini tunaendelea kusimama dhidi yake,” alimalizia Karua akisema mapambano yanaendelea.

Kizza Besigye, kiongozi maarufu wa upinzani nchini Uganda, alikamatwa tarehe 16 mwezi Novemba mwaka 2024 mjini Nairobi, Kenya, na baadaye kuzuiliwa katika gereza la kijeshi mjini Kampala, Uganda.

Anakabiliwa na mashtaka ya uhaini na umiliki haramu wa silaha, akituhumiwa na serikali ya Uganda kwa kupanga njama za kuipindua serikali.

Share This Article