Mwanamuziki wa Rwanda Yeweeh ametangaza ujio wa albamu yake mpya na ambayo ni ya kwanza aliyoipa jina la “Sugar Boi”.
Kazi hiyo ya sanaa inayopangiwa kuzinduliwa rasmi Mei 22, 2026, ina jumla ya nyimbo 16 zinazojumuisha za ushirikiano na zake binafsi.
Yeweeh ambaye awali alikuwa tu mtayarishaji muziki kabla ya kuingilia muziki, atafungua mauzo ya kabla ya uzinduzi ya kazi hiyo Mei 15, 2026.
Albamu hii ina mchanganyiko wa wasanii waliostawi na vipaji vinavyochipuka, wakiwemo Khalfan, Afrique, Papa Cyangwe, Issa, Lina Starz, Confy, Levixone na Lilian Mbabazi kutoka Uganda.
Akizungumza katika mahojiano Yeweeh alisema kuwa mradi huo uliandaliwa kwa makusudi ili kusawazisha uzoefu na sauti mpya.
“Nilitaka kuwapa wasanii wachanga jukwaa huku pia nikileta magwiji. Ilikuwa kuhusu kuunda sauti tofauti na kuchanganya tamaduni,” alisema.
Albamu hiyo inajumuisha nyimbo kama Focus aliomshirikisha Khalfan, Tatata alioimba na Afrique na Papa Cyangwe, Smile alioimba na Lilian Mbabazi na Kirimana ambao ni ushirikiano na Lina Starz.
Ingawa anajulikana sana kwa kazi yake ya utayarishaji, Yeweeh anasisitiza kuwa muziki umekuwa ndoto yake kuu siku zote.
“Mimi kimsingi ni mwanamuziki, hivyo siweki mipaka kwenye kazi yangu. Utayarishaji ulianza kwanza, lakini siku zote nilikuwa na ndoto ya kuwa msanii,” alisema.
Mchakato wake wa ubunifu unaakisi historia yake kama mtayarishaji. Nyimbo nyingi katika Sugar Boi zilikamilishwa kabla wasanii kuingia kuweka sauti zao.
“Msanii angekuja, kusikiliza albamu, na kuchagua kinachofaa mtindo wake,” alisema akisema ni wimbo wa Tatata pekee uliandaliwa kwa ushirikiano kwanzia mwanzo jengwa kwa ushirikiano tangu mwanzo.