Ruto Rais wa kwanza kabisa kuwahi kuhudhuria tuzo za Kalasha

Rais Ruto aliongoza pia katika kuwapa tuzo washindi.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais Ruto akisubiri kumkabidhi mshindi tuzo ya Kalasha

Rais William Ruto jana usiku, aliandikisha historia ya kuwa Rais wa kwanza kabisa aliye madarakani nchini, kuwahi kuhudhuria tuzo kubwa zaidi za uigizaji nchini za Kalasha.

Tuzo za Kalasha ambazo huandaliwa na Tume ya Filamu Nchini, KFC, ziliasisiwa mwaka 2009, hafla ya kwanza ikiandaliwa mwezi Juni mwaka huo, kwa lengo la kutambua vipaji bora katika tasnia ya uigizaji wa filamu na vipindi vya runinga.

Akihutubia waiohudhuria hafla hiyo katika jumba la KICC, kiongozi wa taifa alitangaza kwamba asilimia 30 ya fedha zinazotengewa matangazo ya serikali, itaelekezwa kwenye majukwaa ya ubunifu.

Rais aliongeza kusema kwamba sera hiyo mpya ya matangazo ya serikali inalenga kuongeza uwekezaji katika uchumi bunifu nchini Kenya na hivyo kusaidia na kukuza talanta katika sekta ya filamu.

Huku akipongeza KFC kwa kuandaa tamasha ya filamu iliyohitimika kwa tuzo hizo, Rais alihimiza waandalizi kupeleka tuzo hizo katika magatuzi na kwamba Ikulu itatafuta kuandaa awamu ijayo.

Alielekeza wizara ya fedha kutafuta mbinu za kuwapa waandaaji wa kimataifa wa filamu vichocheo ili waje nchini kuandaa kazi zao, akifichua kwamba hivi karibuni atakutaka na Rais wa Akademia inayohusika na tuzo kubwa zaidi za uigizaji ulimwenguni za Oscar.

Mkutano huo alisema utalenga hasa kuhakikisha kwamba Kenya inatambuliwa ulimwenguni kote kama jukwaa muhimu la ubunifu.

Rais alikuwa ameandamana na waziri wa vijana, uchumi bunifu na michezo Salim Mvurya, Katibu wa masuala ya vijana na uchumi bunifu Fikirini Jacobs na mratibu mkuu wa miradi spesheli ya kirais Dennis Itumbi.

Share This Article