Katika kile kinachoonekana kama jitihada za kusitisha mzozo kati ya Marekani, Israel dhidi ya Iran, Tehran imewasilisha mapendekezo mapya kwenye meza ya mazungumzo.
Kulingana na Shirika la habari la serikali nchini Iran (IRNA), Iran imewasilisha mapendekezo hayo kupitia mpatanishi Pakistan.
Hata hivyo, Shirika hilo halijaweka wazi mapendekezo hayo, lakini hatua hiyo imesababisha bei za mafuta kuanza kushuka.
Wakati huo huo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Esmaeil Baqaei, alisisitiza kuwa Iran umeweka kipaumbele swala la usitishaji vita kwenye mazungumzo na Marekani.
Baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa tarehe 8 mwezi Aprili, Islamabad iliandaa mazungumzo kati ya wajumbe wa Tehran na Washington, ikilenga kuafikia makubaliano ya kumaliza vita vilivyoanza baada ya shambulio la Marekani na Israel dhidi ya Iran tarehe 28 mwezi Februari.