Serikali ya Kenya imelegeza kwa muda masharti kuhusu ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini humo katika juhudi za kuepusha uhaba wa bidha hiyo muhimu.
Hatua hiyo inajiri baada ya usambazaji wa mafuta kutatizika katika taifa hilo la Afrika Mashariki, kutokana na mzozo unaoshuhudiwa katika Mashariki ya Kati.
Kupitia kwa taarifa Alhamisi jioni kwenye ukurasa wa X, Waziri wa Biashara na ustawi wa Viwanda Lee Kinyanjui, alisema wizara hiyo itaruhusu uagizaji wa mafuta ya ubora wa viwango vya chini kwa muda wa miezi sita, hatua ambayo itawawezesha wafanyabiashara kuagiza mafuta hayo, ili kuziba nakisi ya bidhaa hiyo ambayo inashuhudiwa katika baadhi ya maeneo.
“Baada ya tathmini iliyotekelezwa na kamati za kiufundi, na baada ya mashauriano na Shirik la Ubora wa Bidhaa (KBS), na Baraza la Taifa la Ubora, wizara hii ilifanya uchunguzi wa kina kupitia tathmini ya kiufundi,” alisema Kinyanjui.
Hatua hiyo inafuatia hisia za wadau katika sekta ya mafuta ambao wanakumbwa na changamoto kubwa kuagiza mafuta ya viwango vya juu vya ubora kutoka nje.
Hali hiyo inatokana na ugumu wa kusafirisha bidha hiyo kutoka eneo la ghuba ya Hormuz,ambapo asili mia 20 ya mafuta yote husafirishwa.
Kenya imekuwa ikiagiza mafuta ya viwango vya ubora wa hali ya juu kama njia moja ya kuhifadhi mazingira.