Sherehe za mwaka huu za Leba Dei, zinaadaliwa katika shule ya upili ya Chavakali kaunti ya Vihiga.
Kwa mara ya kwanza kabisa tangu Kenya ipate uhuru, sherehe hizo za kitaifa zimeandaliwa nje ya Jiji Kuu Nairobi, huku kaunti ya Vihiga ikiandaa sherehe hizo kwa mara ya kwanza.
Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii Alfred Mutua, alisema matayarisho ya sherehe hizo yamekamilika, ambapo serikali ya taifa imeshirikiana na wadau wengine kuhakikisha ufanisi wa sherehe hizo.
Rais William Ruto, anatarajiwa kuongoza sherehe hizo, huku usalama ukiimarishwa katika eneo hilo.
Wananchi walianza kuwasili kwenye shule hiyo kuanzia saa kumi alfajiri, huku wakiwa na matumaini labda ya nyongeza ya mishahara hususan kutokana na hali ngumu ya maisha inayoshuhudiwa nchini Kenya.
Siku Kuu ya Leba Dei huadhimishwa kutambua mchango mkubwa ambao hutekelezwa na wafanyakazi katika kuchochea ukuaji wa taifa hili kupitia sekta mbali mbali.